Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewapongeza wanahabari ,wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari nchini kwa
kuadhimisha Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani (World Press Freedom Day) leo, Ijumaa, Mei 3, akiwahakikishia kuwa
Serikali yake itaendelea kukuza, kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari
ulioshamiri kwa kiwango cha juu kabisa nchini kwa sasa.
Aidha,
Rais Kikwete amesisitiza kuwa Serikali yake na yeye binafsi, kama mdau wa
habari, wataendeleza kuelekeza nguvu kubwa katika kupanua Uhuru wa Habari kwa
sababu uhuru huo ni kigezo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania
na katika kujenga na kupanua demokrasia nchini.
Katika
salamu zake kwa wanahabari, wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari nchini ambayo
inasherehekea Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Dunia kitaifa mjini Arusha leo
katika shughuli zilizoandaliwa na Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA),
Tawi la Tanzania, Rais Kikwete amesema:
“Kama
muumini na mdau wa Uhuru wa Habari ambao ni sehemu ya Uhuru Mpana Zaidi wa
Kutoa Maoni (Freedom of Expression), napenda kuwapongezeni wanahabari wote
nchini na wadau wenzenu duniani katika kusherehekea siku hii ya kuadhimisha
Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ambayo kitaifa hapa kwetu
inaadhimishwa na shughuli zilizoandaliwa na MISA-Tan mjini Arusha.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais: “Sisi
katika Tanzania tunayo kila sababu ya kusheherekea Siku hii ya leo ya Uhuru wa
Habari nchini kwa sababu sote ni wadau wa habari ni mashahidi wa mafanikio
makubwa na mengi katika nyanja ya habari katika miaka 20 iliyopita katika nchi
yetu. Kwa sababu hiyo, naungana nanyi katika kusheherekea na kuadhimisha
mafanikio haya makubwa.”
Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ambayo
chimbuko lake ni Mkutano wa Waandishi wa Habari wa Afrika waliokutana na kutoa
Tamko la Windhoek (Namibia) – the Windhoek Declaration on Promoting an
Independent and Pluralistic African Press pamoja na kuanzisha Taasisi
ya Habari Kusini mwa Afrika – Media institute of Southern Africa (MISA),
Mei 3, mwaka 1991, ilichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya
Uhuru Duniani mwaka 1993.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Napenda
kutumia Siku hii ya leo kuwapongezeni tena kwa kazi yenu nzuri ambayo imeendelea
kuchangia maendeleo ya nchi yetu kupitia njia ya kuhabarisha, kuelimisha na
kuburudisha wananchi. Vile vile, napenda kutumia nafasi ya Siku ya leo
kuwaelezeeni utayari wa Serikali yetu kuendelea kuithamini kazi hii nzuri. Ni
matumaini yangu kuwa mtaendelea kuifanya kazi yenu kwa kuongozwa na misingi
mikuu ya weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Aidha, kama ambavyo tumekuwa tukifanya, napenda kuwahakikishieni kuwa mimi
binafsi na Serikali ninayoingoza nitaendelea kushirikiana nanyi katika kupanua,
kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari nchini ikiwa ni haki ya waandishi
kufanya kazi yao kwa mazingira mwafaka ya kisiasa, kiuchumi, kisheria na
kijamii. Vile vile, napenda kuwahakikisheni tutaendelea kushirikiana nanyi
katika kulinda uhuru wa wapata habari nchini ambao ni muhimu kama ulivyo uhuru
wa vyombo vya habari.”
No comments:
Post a Comment