Ushirikiano wa pamoja
unatakiwa baina ya wanafunzi, walezi, wazazi, jamii na walimu ili kuweza
kujenga, kuimarisha na kukuza nidhamu , mwenendo na tabia ya mtoto jambo ambalo
litaleta mafanikio chanya pamoja na kutatua changamoto za kitaaluma na kimazingira.
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na
walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Salma Kikwete
iliyopo kata ya Kijitonyama wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema nidhamu ya
mwanafunzi siyo tu kumuamkia mwalimu bali pia kujua wajibu wake kama vile
kuwahi shuleni, kufanya mazoezi ya darasani na kusoma kwa bidii.
“Neno nidhamu lina
dhana pana kwani linagusa wengi lakini katika mazingira ya leo walengwa wakubwa
ni mzazi,mlezi au jamii, mwalimu na mwanafunzi. Kazi ya mzazi, mlezi na
jamii ni kuhimiza na kufuatilia maendeleo ya mtoto.
Mwalimu kufundisha,
kuingia darasani kwa wakati na kujiandaa na kwa mwanafunzi ni
kupokea maarifa anayopewa na mwalimu wake na kusoma kwa bidii”, alisema Mama
Kikwete.
Kwa upande wa wanafunzi
aliwasihi kuongeza juhudi katika masomo na kufanya vizuri kwenye
mitihani, kwani wao na wengine wote wanategemewa na familia, jamii zao na
taifa kwa kuwa watakuwa wakombozi siku za baadaye na kumuomba Mwenyezi
Mungu awape nguvu na ujasiri katika safari yao ndefu ya kufatuta elimu.
Aidha Mama Kikwete
aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya uboreshaji wa
elimu pamoja na kukabiliwa na changamoto kadhaa lakini kadri siku zinavyokwenda
mbele ndivyo Serikali inavyozidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowahusu
walimu.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alisisitiza, “Walimu timizeni wajibu wenu kwa kufika kazini
mapema, kumaliza silabasi kwa wakati, kukamilisha maandalio ya masomo,
kufundisha kila kipindi bila kukosa, kujua taarifa na udhaifu wa wanafunzi wenu
na kuwa kiungo kati yenu na wazazi au walezi hiyo ndiyo nidhamu ya
mwalimu na ndiyo ualimu”.
Akisoma taarifa ya shule hiyo
Mwalimu Elestina Chanafi alisema shule hiyo ilianza mwaka 2007 ikiwa na
wanafunzi 320, walimu 13 na vyumba vya madarasa sita hivi sasa ina wanafunzi
1229, walimu 33 na vyumba vya madarasa 22. Hadi sasa jumla ya wanafunzi
1161 wamehitimu masomo yao tangu walipoanza kutoa kidato cha nne mwaka
2010.
Mwalimu Chanafi ambaye
ni Mkuu wa shule hiyo alisema wamefanikiwa kuchimba kisima cha maji kwa msaada
wa wakorea, kuunganisha umeme, kununua vifaa mbalimbali vya uchapaji na
udurushaji, kuboresha mazingira kwa kiwango cha kutia moyo na kuweza
kuwavutia wanafunzi ili wajisikie kuwa sehemu ya shule.
Kuanzisha maabara ya muda
ambayo imewawezesha wanafunzi wa sayansi kufanya mitihani kwa vitendo na
kuongeza kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo na kupata wanafunzi wa kujiunga na
masomo ya ngazi ya juu kwa idadi nzuri.
“Changamoto zinazotukabili ni
uchakavu wa baadhi ya vyumba vya madarasa, mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao
unasababisha ugumu katika kudhibiti nidhamu ya wanafunzi, uelewa mdogo wa
wazazi juu ya mchango wao kwa maendeleo ya wanafunzi, kiwango kidogo cha ruzuku
toka Serikalini ambacho hakiletwi kwa ukamilifu na wakati, ufinyu wa bajeti na
ulegevu wa uchangiaji wa ada na michango mingine toka kwa wazazi”, alisema
Mwalimu Chanafi.
Naye Mkuu wa wilaya ya
Kinondoni Jordan Rugimbana alimshukuru Mama Kikwete kwa kupata nafasi ya
kuitembelea shule hiyo na kumpongeza kwa kazi anayoifanya ya kuinua kiwango cha
elimu nchini na kuendeleza fani yake ya ualimu kwa faida ya kizazi cha
leo na kijacho kwa kuwasomesha watoto zaidi ya 600 hawa ni mbali na wanafunzi
walioko Shule ya Sekondari WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mama Kikwete
aliichangia shule hiyo mifuko 100 ya simenti ambayo itatumika kuzima
mashimo katika vyumba vya madarasa ambapo wilaya ya Kinondoni itagharamia
mchanga pamoja na kumlipa fundi atakayefanya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment