MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Thursday, October 8, 2015

VIJANA WATAKIWA KUWA MAKINI




Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Vijana wametakiwa kutokubali kutumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa  kwa maslahi ya watu wachache huku hao wanaowatumia wanasonga mbele kimaendeleo na wao wanazidi kurudi nyuma.

Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa  kijiji cha Kikomolela kilichopo  jimbo la Mchinga na mtaa wa Likotwa uliopo Jimbo la Lindi mjini waliohudhuria kampeni ya kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanawatumia vijana kufanya vurugu ambazo hazina  faida katika jamii  zaidi ya kuleta hasara kwani wanaharibu miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara, majengo na hivyo kurudisha maendeleo nyuma.


Kuhusu uchaguzi aliwaomba wananchi wote wa maeneo hayo wakiwemo wanachama wa  vyama vya upinzani kuwachagua wagombea wa CCM ambao watazidi  kuwaletea maendeleo kwani Serikali ya CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, maji na barabara.

“Siku ya uchaguzi ikifika chukua kadi yako ya kupigia kura wahi mapema kituoni kachague viongozi bora utakaoona watakuletea maendeleo na viongozi hawa wanapatikana ndani ya CCM. Msiogope! siku hiyo  kutakuwa na usalama wa kutosha”, MNEC huyo alisisitiza.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Mchinga Saidi Mtanda alisema Serikali ya CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya umeme na katika eneo hilo vijiji 40 kati ya 47 vikiwemo vijiji vya Nangaru na Kitomanga karibu vitawasha  umeme kwa gharama ya shilingi 45,000/=.

Mtanda alisema, “Nawaomba wenzetu kutoka vyama vya upinzani dumisheni  hali ya Amani na utulivu iliyopo kwani kuna baadhi yenu mnatoa  kauli za kuwatisha wanachama wa CCM kitendo ambacho siyo kizuri”,.

Naye mgombea Ubunge wa Jimbo la Lindi mjini Kaunje Selemani aliwaomba wananchi waliohudhuria mkutano huo kumpigia kura ya ndiyo na kuwaahidi kusimamia Ilani ya uchaguzi ya CCM  ambayo itawaletea  maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za  nishati na madini, kilimo, elimu, afya, maji, umeme na barabara.

Katika mikutano hiyo jumla ya wanachama watatu walihama kutoka chama cha Wananchi  (CUF) na kujiunga na CCM.

Wakati huo huo akiwa njiani kuelekea kijiji cha Kikomolela msafara wa Mama Kikwete ulisimama Shule ya Msingi Moka ambapo walimu na wanafunzi walikuwa wamesimama pembeni ya barabara wakiwa wameshika bango lililoandikwa  SHULE YA MSINGI MOKA TUNAUJUMBE KWA MAMA KIKWETE.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo Abdala Mkanjima alimuomba Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni Mwalimu awasaidie kufanya wire ring katika shule yao kwani umeme umepita shuleni hapo.

Mama Kikwete aliahidi kulishughulikia suala la umeme katika shule hiyo. Pia   aliwaasa wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kujikomboa kimaisha na kuwa  viongozi wazuri hapo baadaye ambao watalisaidia  taifa lao na jamii inayowazunguka.


OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YATANGAZA MFUMUKO WA BEI






 Na: Veronica Kazimoto Dar es Salaam
08/10/2015

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2015 umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu Ephraim Kwesigabo amesema kupungua huko kwa mfumuko wa bei kunamaanisha kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2015 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2015.

“Kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2015 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014”, amesema Kwesigabo.

Aidha, Kwesigabo amefafanua kuwa, mwenendo wa bei za baadhi ya  vyakula zilizoonyesha kupungua mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014 ni pamoja na bei za ndizi za kupika kwa asilimia 4.0, matunda (asilimia 2.7), nazi (asilimia 13.3) na mbogamboga kwa asilimia 3.5.

Ameongeza kuwa baadhi ya bei za bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha kupungua mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014 ni pamoja na bei za gesi kwa asilimia 4.9, mafuta ya taa (asilimia 11.7), senti ya sofa (asilimia 5.7), dizeli (asilimia 3.5) na vifaa vya kielektoniki kwa asilimia 1.2.

Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki,  Mfumuko wa Bei nchini una mwelekeo unaokaribiana kwa mfano Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2015 nchini Kenya umeongezeka kidogo hadi asilimia 5.97 kutoka asilimia 5.84 mwezi Agosti, 2015 na Uganda umeongezeka hadi asilimia 7.2 kutoka asilimia 4.80 mwezi Agosti, 2015.

Kupungua kwa mfumuko nwa bei kwa mwezi septemba kumesababishwa na Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 159.04 kwa mwezi Septemba, 2015 kutoka 149.93 mwezi Septemba, 2014. Mfumuko wa Bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwezi Septemba, 2015 umepungua hadi asilimia 9.6 kutoka asilimia 10.2 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2015.



.






 
 









No comments:

Post a Comment