CHAMA cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) imewapatia baiskeli 40 zenye thamani ya Tsh. Milioni 4.8 wahudumu wa afya ya uzazi na ujinsia ngazi ya jamii waliopo katika Kata za Chumbi “A” na Bungu zilizopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Akizungumza Wilayani hapa Ijumaa (Mei 30, 2014), Mkurugenzi Mtendaji, wa UMATI, Bi. Lulu Ng’wanakilala katika hotuba yake iliyosomwa na Meneja Miradi wa UMATI, Bi. Tausi Hassan alisema lengo la kukabidhi baiskeli hizo ni jitihada za taasisi hiyo katika kushirikiana na Serikali ili kuboresha afya ya mama na mtoto na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa Mama na Mtoto kabla na baada ya kujifungua.
Bi. Ng’wanakilala alisema UMATI kupitia ufadhili wa shirika la MERCK Sharp and Dohme (MSD) kutoka nchini Marekani liliweza kupata mradi wa uwiano katika ubunifu wa kuboresha Afya ya Mama na Mtoto, mradi unaotekelezwa katika kwa kipindi cha miaka mitatu katika mikoa ya Pwani na Katavi na kushirikiana kwa karibu zaidi na Ofisi za Mganga Mkuu wa Wilaya.
“Kwa Mkoa wa Pwani mradi huu unatekelezwa katika Wilaya ya Rufiji katika Kata ya Chumbi na Bungu na utekelezaji wake katika maeneo husika ulianza mwaka jana (2013) na miongoni mwa kazi za mradi ni mikutano elimishi kwa jamii, mafunzo ya waelimisha rika, mafunzo kwa wahudumu ngazi ya jamii” alisema Bi. Ng’wanakilala.
Aidha alisema mpaka sasa yapo mafanikio yaliyokwishapatikana tangu kuanza mradi huo katika mkoa wa pwani, hususani Wilaya ya Rufiji ambapo miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na wahudumu 40 ngazi ya jamii wamepatiwa mafunzo na kuanza kazi ya kuhudumia jamii.
Aliyataja mafanikio mengine ni pamoja na vijana 20 waelimishaji rika katika ushiriki wa wanaume masuala ya uzazi na uzazi salama walipatiwa mafunzo na kuanza kutoa elimu kwa jamii. Jamii imeweza kuupokea mradi vizuri na kuonyesha ushirikiano kutoka ngazi ya jamii, Serikali ya Kata/kijiji husika mpaka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya.
Kwa mujibu wa Ng’wanakilala alisema katika mradi huo zipo changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuacha kazi, upungufu wa rasilimali katika utekelezaji wa mradi pamoja na Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ikiwemo mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni nchini ambapo zilileta uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Bw. Rasmo Msabaha alisema Mkoa huo umepanga kufikia asilimia 60 ya malengo iliyojiwekea katika kuzuia vifo vya Mama na Mtoto na hadi kufikia sasa umefikia asilimia 37, na hivyo jitihada za pamoja hazina budi kufanywa katika kufikia kiasi kilichobaki.
“Uzazi wa Mpango ni muhimu sana, hapo zamani Serikali iliweza kutoa bure huduma za afya na elimu, lakini kwa sasa idadi ya wananchi imekuwa kubwa na ndio maana kSerikali imeamua kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo UMATI ili kuweza kusaidia huduma za afya, hivyo ni lazima tuzae kwa mpangilio na kwa kadri tunavyoweza kuwahudumia” alisema
Aidha Msabaha alisema Ofisi yake imejipanga kikamilifu katika kushirikiana kwa karibu zaidi na wahudumu wa afya ya uzazi ngazi ya jamii waliopatiwa mafunzo na UMATI ili kuhakikisha kuwa malengo ya mradi huo yanafikiwa kwa wakati na muda uliopangwa.
Kwa mujibu wa Msabaha aliwataka Wahudumu wa afya ya uzazi kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na UMATI na kufanya kazi walizoelekezwa na Ofisi yake ipo tayari kupokea taarifa ya utelezaji wa mradi huo na endapo kutakuwepo na tatizo lolote Ofisi hiyo ipo tayari kutoa ushirikiano kwa kadri inavyowekana.
Naye Diwani wa Kata ya Bungu, Bw. Ramadhani Mkwaya alisema Ofisi yake imeupokea kwa moyo mmoja mradi huo na ipo tayari kuutekeleza, na akaishukuru UMATI kuichagua Kata yake kati ya Kata 27 zilizopo katika Wilaya hiyo na kusema kuwa hicho ni kielelezo kuwa Kata hiyo inakubalika kimaendeleo.
Aidha Diwani wa Kata ya Chumbi, Bw. Ramadhani Mikole aliwataka wahudumu hao wa afya ya uzazi ngazi ya jamii kutokuwa kimya iwapo kutatokea tatizo la kiutendaji katika majukumu yao, na badala yake wawasiliane mara moja na wahusika wa mradi ili kuhakikisha kuwa mradi unafikia malengo yake.
“Elimu ya siku 9 mliyopewa ni nzuri na pia ni changamoto, iwapo program inaruhusu nawaombeni UMATI muongeze tena siku 9 kwani wahudumu hawa wanafanya shughuli nyingi sana” alisema Mikole.
Mwakilishi wa Shirika la Merck Sharp and Dohme (MSD), Bw. John Nkane alisema shirika hilo ni kampuni ya dawa inayojihusisha zaidi na masuala ya biandamu na imejitolea katika kupambana na vifo vya akina Mama vitokanavyo na uzazi na wameshirikiana na UMATI na kufadhili mradi huo ikiwemo kutoa elimu kwa akina Mama kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki.
“Taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya Akina Mama Wajawazito wanakwenda maeneo yasiyo rasmi, na hivyo shirika letu limejitolea katika kusaidia kuokoa uhai wa Mama na Mtoto, na tumetoa pesa, elimu na kutoa madawa mbalimbali” alisema.
No comments:
Post a Comment